MWANAFUNZI APIGWA RISASI DAR,
Idd Niachieni baada ya kujeruhiwa.
DAR ES SALAAM: Hii haikubaliki! Denti aliyehitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Jitegemee, Idd Niachieni (23) mkazi wa Mtaa wa Madenge, Buguruni jijini Dar, hivi karibuni alitwangwa risasi kichwani na majambazi.Tukio hilo lilitokea hivi karibuni majira ya saa 3 usiku wakati Idd akiwa amekaa na ndugu zake wa kike jirani na nyumbani kwao ndipo majambazi hao walipofika na kuvamia duka lililopo jirani na kwao kisha wakampiga risasi kichwani.
Gazeti la Amani lilifika nyumbani kwao Idd na kuzungumza naye baada ya kupata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitali akawa na haya ya kusema:
“Ilikuwa ni usiku wa saa 3 nikiwa nimekaa barazani kwetu na dada zangu tukipiga stori, ghafla walikuja vijana wawili wa kiume ambao kiumri ni kama ninalingana nao.
…Akionyesha jeraha.
RISASI YA KWANZ YAPIGWA
“Wale vijana walipofika karibu yetu wakaenda kwenye duka la Massawe ambalo linatazamana na nyumba yetu. Ghafla mimi na ndugu zangu tukasikia mlio wa risasi iliyopigwa juu lakini sisi tulihisi mlio huo ni wa baruti tukaanza kuulizana ni nani anapiga baruti?
“Tukiwa hatujapata jibu, alikuja kijana mmoja ambaye alikuwa amevaa kapelo na amejifunga usoni kama ninja, alipofika pale akauliza nyinyi hamuogopi? Akaninyooshe bastola kwenye kichwa changu kisha akasema ondoka,” alisema Idd.
Akizidi kusimulia kwa uchungu, Idd alisema anamshukuru Mungu kwani kama asingeinama kidogo wakati kijana huyo alipomfuata na kumuelekezea bastola, basi ingeweza kumpiga kichwani na pengine angeweza kupoteza maisha hapohapo.
…Akipelekwa hospitali.
IDD ANAENDELEA…
“Sijui nini kilitokea bila shaka ni maamuzi ya Mungu kwani nilikwepesha kichwa kidogo kumbe alikua ameshaiachia risasi ikanipiga kwa kunichuna kichwani. Wale ndugu zangu wakawa wametawanyika wote.
RISASI YACHIMBA UKUTANI
“Baada ya mimi kukwepesha kichwa na risasi ile kunipiga kwa kunichuna ilienda ikapiga ukuta na kuchimba kishimo. Baada ya hapo jamaa huyo alirudi tena katika lile duka.
MUUZA DUKA ATISHIWA, APORWA FEDHA
“Baada ya kurudi pale dukani walimtishia yule muuza duka kisha wakampora fedha amabazo nasikia ilikuwa ni kama shilingi laki 3 au zaidi na vocha ambazo thamani yake haijajulikana kisha wakatokomea sehemu waliyokuwa wameegesha pikipiki yao.
RAIA WATAWANYIKA, MTAA KIMYA
“Kiukweli kutokana na ile milio ya risasi watu wote walitawanyika na mtaa mzima ukawa kimya, nikajikuta niko peke yangu na wale jamaa wakiendelea kufanya mambo yao.
Tundu ilipoingia risasi hiyo.
AKOSA MSAADA
“Kwa mazingira yaliyokuwa ni kama nilikosa msaada kwani watu walikuwa kimya majumbani mwao, nilipojishika kichwani nikagusa damu nyingi sana iliyokuwa ikitiririka, ikabidi nianze kukimbia kuelekea barabara kubwa huku nikiomba msaada.
WASAMARIA WEMA WAMSAIDIA
“Nilipokimbia kwa umbali kama wa dakika kumi au zaidi nikakutana na watu wakiwa kijiweni nikawaomba msaada ndipo wakanisaidia kwa kunipelea Kituo cha Polisi Buguruni, nikatoa maelezo na kufunguliwa jalada namba BUG/RB/5966/2017 UNYANG’ANYI WA SILAA. Kisha wakanipandishwa kwenye bodaboda na kuniwahisha Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu.
ATUNDIKIWA DRIPU 7 ZA MAJI
“Kule hospitalini nilitundikiwa dripu za maji saba kutokana na hali ambayo nilikuwa nayo kwani damu nyingi ilikuwa imemwagika hivyo kulazimika kuwekewa maji mengi mwilini.
ASHONWA NYUZI 15
“Baada ya kutundikiwa dripu za maji nilipatiwa matibabu kwa kushonwa nyuzi 15 kwenye kichwa halafu nikapigwa picha ya X-ray kuangalia kama kuna risasi imebaki au madhara yoyote ya ndani. Nashukuru Mungu majibu ya kipimo kile yalionesha sikuwa na madhara mengine zaidi ya lile jeraha,” alimaliza Idd.
…Akiwa na familia yake.
BINTI ALIYEKUWA NAYE ASIMULIA
Akisimulia mmoja wa dada zake na Idd, Zainabu Niachieni ambaye alishuhudia kaka yake akitwangwa risasi, naye alikuwa na haya ya kusema:
“Tulikuwa tumekaa kifamilia tunapiga stori, ghafla tukasikia mlio wa kwanza ambao tulijua ni wa baruti, wale majambazi wakamsogelea kaka yangu, baada ya hapo nilisikia mlio mwingine kwa ukaribu zaidi, tukatawanyika kila mtu kivyake, lakini baada ya wale watu kuanza kuondoka sikumuona Idd pale ikabidi nianze kumtafuta huku nikimuita.
“Idd alikuwa amevaa fulana nyeupe na mmoja wa wale majambazi alivaa fulana nyeupe. Nikajikuta nataka kuwafuata wale majambazi nikidhani ni Idd. Kiukweli wangeweza kunifyatulia risasi na mimi lakini nikiwa nahaha kumtafuta ndugu yangu, ndipo nikakutana na jirani yetu akaniambia kuwa mdogo wangu kapigwa risasi, damu zinamvuja kwa wingi sana. Tukaelekea alipokuwa.
RISASI MOJA YAOKOTWA
“Wale majambazi walifanikiwa kuokota ganda la risasi waliyopiga juu lakini ile nyingine iliyompiga kaka yangu, ganda lake tuliliokota asubuhi,” alisema Zainabu.
SHUHUDA ASIMULIA
Shuhuda mwingine aliyeshuhudia tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Hadija, naye alilizungumzia tukio hilo:
“Nilikuwa natoka kwenye mihangaiko yangu ndipo nikakutana na Idd akiwa ametapakaa damu nyingi, nilimuuliza akasema amepigwa risasi. Nilimuuliza kama amewajua wale majambazi ndiyo maana walitaka kumuua, akasema hakuna hata mtu aliyemfahamu kwani jinsi walivyokuwa wamejifunika usoni kama maninja,” alisema Hadija.
BABA MZAZI ASHUKURU
Akizungumza na Amani nyumbani hapo, baba mzazi wa Idd, mzee Niacheni alisema tukio hilo limemshtua lakini anamshukuru Mungu kwa kumuepusha mwanaye na kifo.
“Hii ni mitihani ya Mwenyezi Mungu ila kikubwa ninashukuru kuona mwanangu akiwa salama, kwa sababu kama si mpango wa Mungu tungekuwa tunasema mengine,” alisema mzee huyo.
MJUMBE AONGEA
Naye Mjumbe wa Mtaa wa Madenge, Hidaya Mwinyimani alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaasa wenye maduka kukataza makundi ya vijana kwenye maduka yao. Hata hivyo, mjumbe alihimiza suala la ulinzi shirikishi ili kukabiliana na vitendo viovu mtaani kwake.
KAMANDA WA ILALA ATHIBITISHA
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Salum Hamduni alithibitisha kutolea kwa tukio hilo.
“Taarifa za tukio hilo ninazo, ni kweli kuna kijana alipigwa risasi na wahalifu wakati walipokuwa wakipora kwenye duka la huduma ya pesa na vyakula. Upelelezi unaendelea,” alisema.
STORI: GABRIEL NG’OSHA, DAR
No comments