• Breaking News

    Wanafunzi wa fani za afya na Sayansi Kupewa Asilimia 40 ya Mkopo Wote Elimu ya Juu (HESLB) 2017/2018

    Zaidi  ya wanafunzi 30,000 wa vyuo vya elimu ya juu nchini kwa mwaka mpya wa masomo 2017/18, watanufaika na Sh bilioni 427 kutoka Bodi Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), huku wanufaika hao wakiwekwa kwenye mikondo mitatu.

    Jana Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul –Razaq Badru alisema kwa mwaka huu wanufaika wasiopungua 30,000 watapata mikopo ya elimu kulingana na fani walizochagua kusoma.

    Akifafanua idadi na kiwango cha mkopo kitakachotolewa kwa kila mkondo kulingana na fani watakazosoma, Badru alisema bodi imepanga mikondo mitatu ya mikopo. 

    Mkondo wa kwanza unawahusu wanafunzi wa fani za afya, sayansi ya elimu na hesabu, ambapo kundi hilo litapata asilimia 40 ya mkopo huo ambao ni sawa na Sh bilioni 170.8.

    Badru alisema kundi hilo ndilo litapata mkopo mkubwa kuliko makundi mengine kutokana na fani hizo kuwa adimu na zina mahitaji makubwa ya soko nchini hasa kwa kuwapata wataalamu watakaosaidia taifa kwenye sekta za afya, sayansi na elimu.

    Mkondo wa pili umepangwa kupata asilimia 35 ya mkopo wote ambao ni sawa na Sh bilioni 149.45 na wanafunzi watakaonufaika ni wale wa fani za uhandisi, kilimo, misitu, sayansi ya ardhi, usafirishaji na fani kama hizo.

    Mkondo wa tatu umepangwa kupata asilimia 25 ya mkopo wote ambao ni sawa na Sh blioni 106.75 na wanufaika wa mkopo huo ni wanafunzi wote watakaosoma fani za lugha, sanaa, jamii na fani nyingine kama hizo.

    Badru alisema pamoja na bodi kuweka mikondo hiyo, lakini pia suala la jinsia litazingatiwa ili kuepusha jinsi moja kuwa na idadi kubwa ya wanufaika wa mikopo hiyo. 

    Katika hatua nyingine kwa mwezi mmoja uliopita, bodi hiyo imekusanya marejesho ya mkopo ya Sh bilioni 31.1 huku ikiweka mikakati ya mwaka huu ya kukusanya kila mwezi zaidi ya Sh bilioni 14.

    Mtendaji huyo wa HELSB alisema lengo lao ni kuhakikisha wanufaika wote wanafikiwa na kurejesha madeni yao ili yasaidie wengine kupata elimu. 

    Alisema mikakati yaliyojiwekea kuanzia mwaka huu ni kukusanya zaidi ya Sh bilioni 14 kila mwezi na kwamba tangu mwaka huu wa fedha uanze, kwa mwezi Julai pekee wamekusanya Sh bilioni 31.1 huku sekta ya umma ikiongoza kwa wanufaika wake kurejesha madeni yao.

    “Tunakwenda vizuri na tumejiwekea mikakati ya kuhakikisha madeni ya mikopo hiyo yanarejeshwa ili yaweze kunufaisha wengine, kwa sekta ya umma tumefanikiwa kuwafikia asilimia 82 ya wadaiwa wote na sekta binafsi tumefanikiwa kwa asilimia arobaini,” alisema Badru.

    Aliongeza kuwa hivi sasa wameweka nguvu kwenye sekta binafsi, kwa kuwa imekuwa vigumu kuwafikia wadaiwa wote kutokana na sekta hiyo waajiriwa wake kuhamahama kila wakati au kuacha kazi.

    Akizungumzia mikakati ya kukusanya madeni ya mikopo hiyo, Badru alisema wapo mbioni kuanzisha kampeni ya ‘’Kurejesha mkopo ni uzalendo uliotukuka’’, itakayofanywa nchi nzima kuhamasisha wanufaika wa bodi hiyo kujenga tabia ya kurejesha kwa hiari madeni yao.

    Alitaja mkakati mwingine ni bodi hiyo hivi sasa iko kwenye hatua za awali za mazungumzo na taasisi za fedha nchini ili kuona jinsi ya wao kununua mikopo hiyo ya wadaiwa kupitia waajiri wao.

    Awali operesheni ya utafutaji, ufuatiliaji na ukaguzi wa wadaiwa sugu wa bodi hiyo mahala pa kazi yaliyoendesha mapema mwaka huu kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ilifanikiwa kwa kukusanya Sh bilioni 116 ikiwa ni kiwango cha marejesho cha asilimia 46, huku awali walilenga kukusanya Sh bilioni 76.

    Hata hivyo, aliwakumbusha waajiri wote nchini kuhakikisha wanatoa taarifa za waajiri wanaodaiwa na bodi hiyo na kuhakikisha wanakata asilimia 15 ya mshahara yao na kuipeleka bodi ili kulipa madeni yao

    No comments